Translate

Saturday 28 March 2015

Mchungaji Gwajima Ajisalimisha Polisi Kuhojiwa Juu ya Lugha Chafu Dhidi Ya Askofu Pengo.

Mchungaji Gwajima Ajisalimisha Polisi Kuhojiwa Juu ya Lugha Chafu Dhidi Ya Askofu Pengo.


Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, Josephat Gwajima amejisalimisha kituo cha polisi kati kuhojiwa juu ya kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Mchungaji Gwajima anatuhumiwa kumkashifu na kumtukana hadharani Kardinali Pengo. 
Matusi hayo   ni  yale yaliyoonekana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii  ambapo kuna sauti iliyorekodiwa na picha za video zikimuonyesha Mchungaji Gwajima akimkashifu na kumtukana kwa maneno makali Kardinali Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.

Hata  hivyo, mapema  leo  Asubuhi, kipande cha  sauti   ya  Gwajima kilisambaa   katika  mitandao  mbalimbali  ya  kijamii  kikidai kuwa Gwajima angejisalimisha Polisi Jumatatu kwa kuwa kwa sasa yupo Arusha na kuwataka waumini wake kufika polisi Jumatatu bila kufanya vurugu.

Haijafahamika  mara  moja  sababu  zilizomfanya  mchungaji  huyo  Kujisalimisha  leo  Ijumaa.

Hapa chini ni tangazo lilitolewa na polisi kumtaka Gwajima kujisalimisha polisi.
JAMHURI YAA MUUNGANO WA TANZANIÀ
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
PRESS RELEASE
26/03/2015
ASKOFU GWAJIMA ATAKIWA KUHOJIWA NA JESHI LA POLISI KUHUSU TUHUMA ZA KASHFA NA MATUSI DHIDI YA KALDINARI PENGO.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtaka Askofu JOSEPHAT GWAJIMA wa Kanisa la Ufufuo na Uzima afike haraka katika kituo cha Polisi cha Kati ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kashfa na matusi.
Tumepokea malalamiko ya kukashifiwa na kutukanwa hadharani Mwadhama Kaldinari Polycarp Pengo ambaye ni kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile WhatsApp na mingineyo kuna sauti iliyorekodiwa (audio) na picha za video (Video Clip) zikimuonyesha Askofu Gwajima akimkashfu na kumtukana kwa maneno makali Kaldinari Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.
Baada ya tukio hilo juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika hali ya kawaida ili kumpata Askofu Gwajima bila mafanikio na hivyo yeye mwenyewe sasa anatakiwa aende akaripoti haraka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam bila kukosa.
Ni muhimu sana kwa Askofu Josephat Gwajima kuripoti yeye mwenyewe badala ya Kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii.
Jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri hili unaendelea ili sheria. ichukue mkondo wake.
S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments: