Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza alisafiri hadi mjini Eldoret ambako shahidi muhimu wa upande wa mashitaka katika kesi inayomkabili naibu Rais wa Kenya Meschak Yebei aliuawa.
Alikutana na familia ya marehemu Yebei.
“Singeweza kuutizama mwili wake tena;uikuwa na majeraha mabaya…hata sikuweza kumtambua mara ya kwanza, “ alinieleza mkewe Meschak Yebei nje ya chumba cha kuhifadhia maiti, katika mji wa Eldoret, Kaskazini mwa Kenya
Lilian Yebei alisema kuwa mumewe, ambaye alikuwa akitarajiwa kutoa ushahidi katika mahakama ya kimataifa ya ICC, alitoweka siku 10 zilizopita.
Maiti yake ilipatikana mwishoni mwa juma takriban kilomita 40 (Maili 25) kutoka nyumbani kwake. Ilikuwa imekwama katikati ya mawe kwenye mto.
Haijabainika ni nani aliyehusika na mauaji hayo- Maafisa wa usalama wanasema wameanzisha uchunguzi.
Lakini familia yake inaamini kuwa aliuawa kutokana na uhusiano wake na mahakama ya ICC. Hata hivyo taarifa mpya zimejitokeza kusema kwamba Yebei alihusishwa na juhudi za kuwahonga mashahidi katika kesi inayoendelea katika mahakama ya ICC kuhusu washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi.
Viongozi wa mashitaka wanasema kuwa hawakutarajia kumwita tena bwana Yebei kutoa ushahidi kwa sababu ya hilo.
Na licha ya mauaji yake kuwa ya kikatili, sio ya kipekee kushuhudiwa jijini Eldoret, ambako kulishuhudiwa ghasia mbaya zaidi baada ya uchagzi wa mwaka wa 2007
Wale wanaoaminika kuhusika na ghasia hizo wameshtakiwa katika mahakama ya ICC
Familia kadhaa zimeripoti kutoweka kwa wao katika mazingira ya kutatanisha. Wengi walionekana kuwa mashahidi katika mahakama hiyo iliyoko Hague Uholanzi.
Mwezi uliopita, Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda alisema kuingiliwa kwa mashahidi na kutishwa kwao kulichangia katika kusambaratika kwa kesi iliokuwa ikimkabili Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Baadhi ya mashahid wa upande wa mashtaka walikuwa wamebatilisha ushahidi wao na wengine wakatoweka katika hali ya kutatanisha.
'Uchunguzi wa ICC Kenya'
Lakini matatizo kuhusiana na mashahidi hayakuanza hivi majuuzi. Yamekuwepo tangu ICC ilipoanzisha uchunguzi wake mwaka 2010/11.
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yalishutumu serikali ya mseto iliyoingia mamlakani baada ya uchaguzi w mwaka 2007 na serikali ya sasa kwa kutoshirikiana na ICC-madai ambayo serikali zote mbili zimekanusha
ICC awali iliwafungulia mashtaka watu sita kutoka pande zote mbili za kisiasa mwaka wa 2007. Kati ya hao 6, ambao wote wamekanusha madai hayo, ni wawili tuu ambao sasa wanakabiliwa na mashtaka.
Lakini je ni kwa nini miongoni mwa kesi zote za ICC, ni mashahidi nchii Kenya, ambao wameingiliwa sana?
Labda jibu ni kuwa kesi ilihusisha watu mashuhuri ambao walikuwa na wafuasi wengi.
Mahakama ilitambua hayo na iliitaka serikali kuwalinda zaidi mashahidi kutoka pande zote mbili
Bwana Yebei, alitambuliwa kama shahidi mara ya kwanza mwaka wa 2011, pale mwanablogu mmoja mashuhuri ambaye sasa anafanya kazi ikulu, alipofichua barua pepe iliyokuwa na majina kadhaa ya mashahidi
'Yebei aliishi kwa uoga'
ICC ilikasirishwa sana na hatua hiyo na kuahidi kuchukua hatua. Lakini hakuna lolote lilifanyika. Washtakiwa wote katika kesi hiyo wamekanusha madai ya kuhitilafiana na mashahidi.
Lakini tangu wakati huo, familia ya Yebei inasema amekuwa akiishi kwa uoga.
Ameripoti mara kadhaa kwa polisi kuhusu kupokea vitisho kutoka kwa watu aliowafahamu, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Familia yake imehama mara mbili katika eneo la Uasin Gishu, kuepuka kupatikana, kasha Yebei akaamua kuwaacha nyuma na kupokea ulinzi wa ICC.
Mawakili wa naibu wa Rais William Ruto ambaye ameshtakiwa pamoja na mtangazaji Joshua Sang, wanasema Yebei alikuwa shahidi muhimu sana katika kesi yake.
Anatoka kabila sawa na Ruto, lakini wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2007 alikuwa mratibu katika chama pinzani.
'Siasa za Kenya'
Siasa nchini Kenya huegemea kabila, na kwa hiyo tayari alikuwa amejiweka tofauti na jamii yake. Licha ya haya familia inasema alikuwa na uhusiano wa karibu na Ruto.
Nyumba ya Yebei haiku mbali na ile ya Bwana Ruto – Familia yake wanasema iko umbali wa mita chache tuu kutoka kwao.
Taarifa ya ICC inasema Yebei alikuwa chini ya ulinzi, ikiwemo kupewa “makao salama katika eneo jipya”, lakini haijui ni kwa nini alirejea Eldoret.
Familia yake inasema ilikuwa kumwona mwanawe mgonjwa na mkewe, ambaye anatarajiwa kujifungua mwezi Februari.
Alinionesha picha za familia wakiwa pamoja likizoni
Yebei, mwenye umri wa miaka 34, alijikimu maishani kwa kununua na kuuza nafaka kama vile mahindi, na pia alikuwa katika siasa- waliokuwa karibu naye wanasema hakuyumbishwa kwa urahisi, hata iwapo msimamo wake haukupendwa." Alikuwa mtu mzuri, na mpatanishi, na sijui kwa nini yeyote angetaka kumuua,”anasema mjane wake. "Nimwewachwa mapema sana”
Kifo chake kimekuwa mada ya mazungumzo katika mji wa Eldoret na kwingineko
Maswali magumu pia yangalipo kuhusu juhudi za polisi kumsaka baada ya kutoweka kwake 28 Desemba, huku kukiwa na madai kuwa haikutekekelezwa ipasavyo. Pia kuna shauku kuhusu iwapo
waliomuua watapatikana na kubaini ni kwa nini.
Polisi hawajazungumzia kesi hii, ila tuu wamesema kuwa uchunguzi unaendelea.
Lakini huku kesi dhidi ya Naibu rais ikianza tena mwezi huu huko the hague, usalama wa mashahidi utaangaziwa , kwa mara nyingine tena
Familia ya Yebei inahisi kwamba imetamaushwa na maafisa wa usalama na mahakama hiyo ya ICC.
Wanasema licha ya kuwa maisha yake kuwa hatarini, vitisho dhidi yake havikutiliwa maanani.
No comments:
Post a Comment