Meya wa Jiji Dar atia kiwewe vigogo
(Mwanahalisi) DAHIRA ya Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam kukamata wakwepa kodi na kuwafikisha mahakani inatia kiwewe vigogo wengi, anaandika Happyness Lidwino.
Amesema, amepanga kukamilisha mambo mengi katika kipindi cha miaka mitano kwenye nafasi hiyo lakini donda ndugu la ukwepaji kodi atashughulika nalo kwa kuwa, limeota mizizi ndani ya jiji hilo.
Akizungumza na mtandao huu jana Mwita ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Vijibweni (Chadema) amesema, vigogo wakwepa kodi wanapaswa kujua kuwa “huu ni utawala mpya wenye lengo la kurudisha maendeleo kwa watu wote bila upendeleo.”
Amesema, licha ya jiji hilo kuwa na vyanzo vingi vya mapato bado wananchi wake wanaishi maisha duni kutokana na baadhi ya vigogo wenye biashara nyingi kutolipa kodi ipasavyo.
“Nasubiri tu wiki ijayo niapishwe ili nianze kuwafuatilia wote wenye viporo vya kodi na wanaokwepa.
“Nina mipango mingi ya kimaendeleo lakini yote inahitaji pesa ambazo ni lazima zipatikane kwa njia ya kodi na kuongeza vyanzo vya mapato,” amesema Mwita.
Amesema kwamba, kwa muda mrefu amekuwa akitamani kuwa meya wa jiji ili aweze kuweka wazi uozo wa utawala uliopita.
“Mimi pia ni mmoja kati ya wananchi waliotoka katika familia ya kimaskini, kwa hiyo ninatambua shida za wananchi ambapo nikianza kazi kwa kushirikiana na mameya wa wilaya, zitatatuliwa,’’ amesema.
Changamoto nyingine kubwa katika jiji hilo Mwita anataja kuwa ni uchafu uliokithiri. “Nina mpango wa kujenga dampo kubwa kila wilaya ili kuondoa taka zinazozagaa jijini kwa kusubiri kukusanywa na kupelekwa dampo kubwa la pugu.
“Ninaamini kwa kufanya hivyo suala la taka kuzagaa kila mahali itakuwa ni ndoto,” amesema Mwita.
Hata hivyo ameahidi kutatua kero ya foleni ya magari kwa kujenga maeneo ya maegesho ya magri katika kila wilaya ili kusaidia wafanyakazi huegesha magari yao nyumbai na kwenda katika shuguli zao kwa daladala.
Akizungumzia uhaba wa vyoo vya umma Mwita amesema asilimia kubwa katika sehemu muhimu zinazokaliwa na watu wengi hakuna vyoo vya bure.
“Hii nayo ni kero kwa namna moja ama nyingine kwani vipo vya kulipia tu hakuna vya bure na hata kama vikiwepo havina ubora. Na kuna wengine pia hawana uwezo wa kujilipia huduma hiyo. Hili litakuwa ni jambo la haraka kushuhulikiwa,” amesema Mwita.
No comments:
Post a Comment